Friday , 20th Mar , 2015

Kocha Amri Said 'Stam' ameanza kazi ya kuinoa Polisi Morogoro akitokea Mwadui FC ya Shinyanga baada ya Uongozi wa timu hiyo kumsimamisha aliyekuwa kocha Mkuu Adolf Richard.

Amri aliyewahi kukipiga Simba, anatarajia kuungana na Jamhuri Kihwelo 'Julio' ambaye bado anafanya mazungumzo na uongozi wa Polisi Morogoro ambapo Wawili hao ndiyo walioipandisha Mwadui FC kutoka ligi daraja la kwanza hadi ligi kuu.

Katika taarifa yake, Msemaji wa Polisi Moro, Clement Bazo amesema wapo katika mazungumzo na Julio na bado hawajafikia muafaka ila Amri Said ameshaanza kazi katika kikosi hicho na yuko na jijini Mbeya ikijiandaa na mechi yake dhidi ya wajelajela Tanzania Prisons.

Polisi ilimsimamisha kocha wake Adolf mapema mwezi huu baada ya kutoka sare ya kutofunga na Ruvu Shooting kwenye mchezo wa ligi kuu Tanzania bara, mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.