Monday , 15th Feb , 2016

Aliyekuwa mkuu wa shirika la kupambana na madawa ya kuongeza nguvu mwilini nchini Urusi RUSADA, Nikita Kamaev ameaga dunia

Aliyekuwa mkuu wa shirika la kupambana na madawa ya kuongeza nguvu mwilini nchini Urusi RUSADA,Nikita Kamaev ameaga dunia.

Kamaev ameaga dunia yapata miezi miwili pekee tangu ajiuzulu kufuatia ufichuzi wa shirikisho la riadha duniani kuhusu matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu mwilini miongoni mwa wanariadha wa nchini Urusi.

Shirikisho la riadha la Urusi RUSADA limesema kuwa Kamaev alikumbwa na mshituko wa moyo, huku likiandika "Marehemu atasalia katika kumbukumbu zetu kutokana na uadilifu wake na maono yake'' taarifa hiyo ya RUSADA ilieleza.

''Kamaev alilalamikia maumivu ya moyo baada ya kushiriki mchezo wa kuteleza kwenye barafu'' Alisema mkurugenzi wa zamani wa Rusada jenerali mstaafu Ramil Khabriev.

Kifo chake kimetokea wakati ambapo Urusi imepigwa marufuku ya kutoshiriki mashindano yeyote ya riadha na kamati ya olimpiki duniani IOC na shirikisho la riadha duniani IAAF.

Kamaev alijiuzulu ili kuruhusu uongozi wa RUSADA kuweka mikakati mipya ya kuirejesha katika mashindano ya kimataifa ya riadha ikiwemo michezo ya Olimipiki ya yatakayoandaliwa Agosti mwaka huu huko Rio de Jenairo nchini Brazil.