Monday , 26th Mar , 2018

Golikipa namba moja wa timu ya taifa ya Tanzania Aishi Manula ataukosa mchezo wa kirafiki wa kesho dhidi ya DR Congo ambao utapigwa kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es salaam.

Kocha msaidizi wa Taifa Stars Hemd Morocco ameweka wazi kuwa hali ya mlinda mlango huyo wa vinara wa ligi kuu Simba, bado si nzuri hivyo katika mchezo wa kesho hatacheza badala yake watamtumia Mohamed Abdulrahman.

Kwa upande mwingine Morocco amesema mechi ya kesho itakuwa ngumu kwani wanahitaji kushinda ili kujiweka vizuri kwenye viwango vya FIFA lakini ana matumaini mechi itakuwa nzuri.

Naye kocha wa timu ya taifa ya DR Congo Florent Ibengé amesema anatarajia kupata ushindani mkubwa kutoka kwa taifa Stars kwani wametoka kupoteza mchezo wao dhidi ya Algeria hivyo anaamini hawatakubali kupoteza kirahisi.

DR Congo inashika nafasi ya 39 kwenye viwango vya ubora vya FIFA duniani kwa mwezi Februari wakati Tanzania ikiwa inashika nafasi ya 146 kwa mwezi Februari. Kuna uwezekano mkubwa Tanzania ikapanda endapo itapata ushindi kwenye mechi ya kesho.