Tuesday , 17th Nov , 2015

Kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania Bara,Kilimanjaro Stars, Alhaj Abdallah Athumani Seif 'King Kibadeni' ametangaza kikosi cha wachezaji 21 kujiandaa na michuano ya Kombe la Chalenji itakayoanza kutimua vumbi Jumamosi Novemba 21, nchini Ethiopia.

Kibadeni anayesaidiwa na kocha msaidizi Juma Mgunda, amesema wachezaji aliowaita wapo katika hali nzuri na wamekuwa wakifanya mazoezi na kikosi cha Taifa Stars ambapo wao kama benchi la ufundi wamepata nafasi ya kuwa nao kwa muda mrefu na kutambua maendeleo yao.

Wachezaji walioitwa ni makipa, Ally Mustafa (Yanga) na Aishi Manula (Azam), Said Mohamed (Mtibwa Sugar). Mabeki Shomari Kapombe (Azam), Hassan Kessy (Simba), Mohammed 'Tshabalala' Hussein (Simba), Hassan Isihaka (Simba), Salim Mbonde (Mtibwa), Juma Abdul (Yanga) na Kelvin Yondani (Yanga).

Viungo Himid Mao (Azam), Jonas Mkude (Simba), Said Ndemla (Simba), Salum Telela (Yanga), Salum Abubakar (Azam), Deus Kaseke (Yanga), washambuliaji John Bocco (Azam), Elias Maguri (Stand United), Ibrahim Hajibu (Simba), Malimi Busungu (Yanga) na Saimon Msuva (Yanga).

Michuano ya Kombe la Chalenji inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Novemba 21 na kumalizika Desemba 6, ambapo Kilimanjaro Stars imepangwa kundi A, lenye wenyeji Ethiopia, Rwanda na Somalia.

Wachezaji Said Mohamed, Juma Abdul, Hassan Kessy, Hassan Isihaka, Salum Abubakar na Ibrahim Ajibu wanaendelea na mazoezi jijini Dar es salaam chini ya kocha msaidizi wa Kilimanjaro Stars, Juma Mgunda wakati wanawasubiri wachezaji wengine walioko nchini Algeria na kikosi cha Taifa Stars.

Wachezaji hao wamechaguliwa katika kikosi cha Kilimanjaro Stars kitakachoshiriki michuano ya Chalenji itakayofanyika nchini Ethiopia ambapo Tanzania imepangwa kundi A ikiwa na timu mwenyeji wa michuano hiyo Ethiopia, Rwanda na Somalia.

Kundi B lina bingwa mtetezi Kenya, Burundi, Uganda na Zanzibar, huku kundi C likiundwa na timu za Sudan, Sudani Kusini, Djibout na waalikwa wa michuano hiyo timu ya taifa kutoka Malawi.