Makocha wa Serengeti Boys, kutokea kushoto ni Muharami Mohammed, Bakari Nyundo Shime na mshauri wa benchi la ufundi, Kim Paulsen wakiwa nchini Congo.
Shime maarufu kama Mchawi Mweusi, amezungumza hayo wakati anaendelea kufanya maandalizi ya mwisho ya mchezo dhidi ya Jamhuri ya Congo utakaofanyika Jumapili Oktoba 2, kwenye Uwanja wa Alphonse Massamba-Débat ulioko kwenye Makutano ya Barabara za Nkolo na Boko, hapa jijini Brazzaville.
Katika mazungumzo yake, Shime anasema: “Timu iko vizuri. Tumejiandaa vizuri kwa yale ya msingi yote tumekamilisha. Kwa hivyo, kila kitu kiko sawa, kama tulivyokusudia. Tupo hapa Congo kwa sasa kumalizia au kukumbushia mambo mawili au matatu hivi" Amesema Shime
Shime amesema kwamba mfumo atakaoutumia ni wa 4-4-2 katika mchezo huo wa kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana. Fainali hizo zitafanyika jijini Antananarivo, Madagascar mwezi Aprili, mwakani.
Anasema kwamba mfumo huo ni rafiki kwa Serengeti Boys kwani katika michezo takribani 15 ya kimataifa hajapoteza hata mmoja, “Kwa hivyo siwezi kubadili mfumo huu. Ni mfumo wa kushambulia na kulinda tusifungwe. Vijana wanauelewa zaidi na ndio mfumo wetu.”
Akiwaelezea Congo - wapinzani wake, Kocha Shime anasema: “Ni timu ya kawaida kwa maana wanafungika. Kwenye mchezo huu ukiangalia kwa makini sisi ndiyo tunahitaji zaidi ushindi kuliko Congo. Lakini nataka uwaambie Watanzania kwamba pamoja na hayo, nawaheshimu Congo, najua wako nyumbani lakini mwisho wa siku ni wachezaji 11 kila upande ndio watakaoingia uwanjani.”
Amesema kwamba amekiandaa kikosi chake vema kabisa katika eneo la mbinu, ufundi na saikolojia. “Akili za vijana wangu wooooote ni kuhakikisha tunafanya vema kwenye mchzo wa Jumapili.”
Naye Kocha wa Makipa, Muharami Mohammed au Shilton, alisema: “Silaha zangu ziko tayari kwa vita, makipa wangu wangu wote akiwamo Kelvin Kayego, Ramadhani Kabwili na Brazio wote wako fiti. Ye yote kati yao anaweza kucheza.”