Katibu Mkuu wa CHADEMA Dkt. Vincent Mashinji
Amesema amesema kwa sasa chama hicho kinaendelea na kazi zake za kujiimarisha kila kona nchini na kuwatetea wananchi katika masuala mbalimbali ya maendeleo.
Dkt. Mashinji ameyasema hayo katika kipindi cha KIKAANGONI kinachorushwa na EATV kupitia ukurasa wake wa Faceebook, wakati akijibu maswali ya wananchi.
Amesema chama hicho kimeanza mikakati ya kushinda uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020 na kuwataka wananchi kuendelea kukiunga mkono chama hicho na kubainisha kuwa kwa sasa wameanza kuwekeza nguvu vijijini ili kuhakikisha chama kinasikika kuanzia ngazi ya msingi wa familia.
“Wananchi wanauliza kwamba tumepoa, siyo kweli ukimya wetu una kishindo , tunajipanga kufanya mambo mbalimbali na mikakati hiyo siyo vyema kuiweka hapa, lakini hivi karibuni wananchi wataona uwakilishi wetu kwao, CHADEMA ipo imara” Amesema Dkt. Mashinji.
“Tunajipanga kukamata dola mwaka 2020 na tunawaomba watanzania kuendelea kutuunga mkono kwani nia yetu ya kuiongoza taifa hili kuwa na uchumi imara na kuhakikisha maisha ya wananchi yanaimarika upo palepale” Amesema Mashinji.
Aidha Mashinji amesema Baraza la Vijana la CHADEMA ,BAVICHA na Baraza la Wanawake BAWACHA wote wamejipanga vizuri katika kuhakikisha kwamba chama kinaenea kwa wananchi kuanzia ngazi ya chini.
Aidha Mashinji amesema CHADEMA huwa haisusii vikao halali ambavyo huwakutanisha na chama tawala CCM ila pale ambapo huona vikao husika havina nia ya kutaka kutenda haki ndipo hujitoa katika vikao hivyo na kuwataka wananchama kuendelea kuwa na imani na chama hicho.