Friday , 9th Dec , 2016

Mashabiki wa sanaa nchini na Afrika Mashariki leo Jumamosi ya Desemba 10 watapata kujua wasanii wa muziki na filamu watakaoibuka washindi wa tuzo kubwa kuwahi kufanyika nchini na Afrika Mashariki kwa ujumla za EATV Awards 2016.

Muonekano wa Stage

 

Tuzo hizo ambazo zimeandaliwa na kituo namba moja kwa sasa nchini Tanzania cha East Africa Television (EATV) Ltd, zinalenga kuboresha kazi za Sekta ya Sanaa, zinatolewa kwa wasanii mbalimbali wanaojihusisha na sanaa katika kutambua mchango wao pamoja na ubora wa kazi zao.

Lengo la kuanzisha Tuzo za EATV ni katika kuhakikisha kuwa kunakuwepo na ushindani katika Sekta ya Sanaa Afrika Mashariki ili kusaidia kuziboresha viwango vyake na kuwa na kazi nzuri zenye ubora unaoweza kushindanishwa kimataifa.

Hafla ya utoaji tuzo za EATV, zitafanyika katika ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mh. Nape Moses Nnauye.

Kwa mwaka huu jumla ya wasanii 45 wanawania tuzo za EATV katika vipengele tisa tofauti ambavyo ni vya Mwanamuziki Bora wa Kiume, Mwanamuziki Bora wa Kike, Wimbo Bora wa Mwaka, Video Bora ya Mwaka, Kundi Bora la Mwaka, Mwanamuziki Bora Chipukizi, Muigizaji Bora wa Kiume, Mwanamuziki Bora wa Kike, Filamu Bora ya Mwaka pamoja na Tuzo ya Heshima.

Bei ya tiketi ni Shilingi 20,000 kwa 50,000 endapo utanunua katika vituo vya mauzo lakini endapo utanunua kwa njia ya M Pesa, tiketi zinakuwa ni shilingi 18,000 na shilingi 45,000/-

Utoaji wa tuzo za EATV Awards utaambatana na burudani murua kutoka kwa wasanii wakali kama vile Barnaba Boy, Maurice Kirya kutoka Uganda, rapa mkali Darassa, Shetta, Vanessa Mdee, Wahu kutoka Kenya, Lady JayDee, Ali Kiba aka King Kiba pia Madansa wakali wa shindano la kudansi la Dance100% 2016, washindi Team Makolokocho, Clever Boys pamoja na D.D.I

Tuzo za EATV zinadhaminiwa na Vodacom, Coca Cola, Benki ya Barclays na Africasongs

Tags: