Friday , 16th Oct , 2015

Producer DX kutoka studio za Noise Maker zilizoko mkoani Arusha, amewataka producer wengine wakubwa walioko mikoani kutokimbilia kufanya kazi zao jijini Dar es salaam, kwani kwa kufanya hivyo kunawanyima fursa wasanii wazuri walioko mikoani.

DX ameongea na Planet Bongo ya East Africa Radio, na kusema kwamba kufanya hivyo sio kutatua tatizo kwani hata hao wasanii wa mikoani, wanahitaji producer wazuri.

"Tumejifunza mengi kutoka kwa wadau ambao wako Dar es salaam na wasanii wakongwe, tunaamini kwamba maendeleo hayaji kwa kukimbia tatizo, bali kwa kukabiliana nayo, kwa hiyo sisi kama Noise Maker Productio Studios kwa miaka kadhaa tumeweza kujitahidi na tumeona mafanikio ya kwamba tukiweza kujikita huku nyumbani tutaleta maendeleo, tutaweza kuwasaidia wasanii wa huku nyumbani waweze kuwa na muono tofauti wa kisasa juu ya tasnia ya muziki", alisema DX.

DX aliendelea kwa kusema kwamba nchi yetu ina rasilimali nyingi na kila mkoa una ladha yake katika muziki, lakini Dar es salaam wanaichukulia kama kituo cha kuutangaza muziki kimataifa.

"Tanzania kwa namna ilivyo ina rasilimali nyingi sana, na rasilimali hizo ziko katika mikoa mbali mbali, hivyo pia vipaji vya muziki au vipaji vya sanaa vipo vingi na katika kila mkoa kuna ladha yake, kwa hiyo Dar es salaam tunaichukulia kwamba ndio kitovu cha kuvitangaza zaidi na hatimaye kuingia katika soko la kitaifa hata kimataifa", aliendelea kusema DX.