Tuesday , 9th May , 2017

Nikki wa Pili amefafanua kauli yake ya uchunguzi wa ajali ufanyike, na kusema ni jambo la utu kama tatizo litajulikana na kufanyiwa marekebisho kwa vitendo na siyo kuhukumu watu au kumtafuta mchawi nani kipindi hiki, huku akitaka asinukuliwe vibaya.

Akizungumza jana kwenye Planet bongo ya East Africa radio, Nikki amesema kuwa lengo la yeye kuomba mamlaka husika kufanya uchunguzi alihitaji wananchi wote kwa ujumla waweze kujifunza kupitia ajali hiyo, na kwamba kama itawezekana wakati mwingine tatizo hilo lidhibitiwe mapema.

"Nasikitika watu wameninukuu vibaya sana niliposema uchunguzi ufanyike wengine wameniponda lakini sijachukia kwani hawajanielewa. Uchunguzi ukifanyika sina maana ya kumhukumu mtu mmoja hapana bali tuweze kujifunza. Watu wengi waliokusanyika uwanjani kuaga walimu na wanafunzi wameonyesha utu lakini pasipo tukio hili kuchunguzwa utu wao utakua hauna thamani kwani matatizo haya yatajirudia mara kwa mara"-.alisema Nikki.

Hata hivyo Nikki ameongeza kwamba "Inawezekana kuwa mikanda ilikosekana kwenye 'bus' walilokuwa wamepanda wanafunzi na walimu wa Lucky Vicent Academy au mwendo haukuwa mzuri lakini tatizo linaweza kuwa hali ya hewa hivi ni vitu ambavyo vikifanyiwa uchunguzi vinaweza kutukumbusha tabia zetu na tutajifunza wakati mwingine"-aliongeza Nikki wa Pili.

Katika hatua nyingine Nikki ametumia muda wake kwenye Planet Bongo kuwaonya watu wanaoweka mitandaoni picha za ajali na kusema kuwa ni vitendo vya udhalilishaji na kuongeza kwamba zipo njia nyingi za kutoa taarifa kwenye mitandao lakini siyo kwa ku- 'share' picha za ajali ambazo watu wanakuwa wameumia vibaya