
Kitendo cha wasanii kutoa wimbo mmoja badala ya albamu iliyokamilika, ni moja ya sababu inayopelekea Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kushindwa kuzipitia na kukagua nyimbo hizo, kwani mfumo uliopo ni wa kukagua albamu iliyokamilika.
Taarifa hiyo imetolewa na Afisa habari wa BASATA Aristide Kwizela, alipokuwa akiongea kwenye kipindi cha Planet Bongo kinachorushwa na East Africa Radio, na kusema kwamba sasa hivi kazi zinazohakikiwa ni zile zilizopo kwenye albam, na kwa upande wa wimbo mmoja mmoja, bado haujawekwa mfumo maalum wa kukagua.
"Kwa sasa hivi kazi ambazo zina hakikiwa ni zile ambazo zipo kwenye mfumo wa albam, lakini inapokuwa ni singo, bado mechanism hii haigusi eneo hilo, urasimishaji haugusi kuikagua single moja moja, utaona kwamba sasa hivi wasanii wa muziki wa kizazi kipya, wengi hawatoi albam, wamekuwa watu wanaotengeneza singo moja moja, anatafuta show na ndio pato lake linatokea kwenye hiyo singo", alisema Kwizela.
Pamoja na hayo Bwn. Kwizela amesema msanii anatakiwa asajiliwe na BASATA ili atambuliwe ni msanii anayefanya kazi za sanaa, na anatakiwa kabla hajapeleka albam au kazi yake sokoni, ni lazima ipelekwe na kuhakikiwa na Baraza la Sanaa la taifa, pamoja na Bodi ya Filamu ya Taifa.
"Msanii anapaswa kusajiliwa na Baraza la sanaa la taifa ili kwanza atambuliwe kuwa ni msanii na anafanya kazi za sanaa, kwa sasa hivi baada ya serikali kurasimisha sekta ya sanaa, msanii yeyote kabla hajapeleka albamu yake sokoni, ni lazima kazi yake ihakikiwe na BASATA kwa wale wanaofanya muziki, kwa wale wanaofanya filamu kazi zao inabidi zihakikiwe na bodi ya filamu, pamoja na video zinazozalishwa na wasanii wa muziki, kwa hiyo msanii anapotoa video kazi zake lazima zihakikiwe na Bodi ya Filamu, na audio ni lazima ihakikiwe na Baraza la sanaa la Taifa", alisema Kwizela.