Wednesday , 31st Jan , 2018

Msanii wa Singeli Bongo maarufu kwa jina la Manfongo amesema sasa hivi anapata usumbufu mkubwa kutoka kwa familia ya marehemu Mbaraka Mwinshehe, ambaye ametumia kionjo cha wimbo wake.

Akizungumza kwenye Planet Bongo ya East Africa Radio, Manfongo amesema watoto wa marehem Mbaraka Mwinshehe wamekuwa wakimfuata kudai fidia ya yeye kutumia kazi ya baba yao, lakini kila mmoja anakuja kwa muda wake na documents zake.

“Sasa hivi nasumbuliwa sana na familia ya Mbaraka Mwinshehe, wanataka milioni saba, wananisumbua wale watoto, mimi nimetoa ngoma kwa mapenzi ili mradi kuutangaza mziki wa singeli, mwanzo watu walikuwa wanauona kama uhuni, nikaona ngoja nichukue ngoma hata za miaka 90 nichanganye, hata mzee akikaa na wanawe wanaweza sema kumbe wanafanya kitu kizuri, na sio kwa nia mbaya, na wapo watoto wawili wanaonifuataga, kila mmoja anakuja na documents zake kuonyesha yeye ndio mmiliki”, amesema Manfongo.

Pamoja na hayo Manfongo amesema bado hajaingiza pesa kubwa kupitia pesa hiyo, kwani kazi ndio kwanza imeingia mtaani na muziki wake haujaanza kumlipa kwa kiasi kikubwa, hivyo bado anajichanga changa aweze kulipa.