Saturday , 25th Aug , 2018

Msanii wa bongo fleva, Beka Flavour amedai yupo katika mpango wa kuzungumza na Aslay Isihaka kwa lengo la kutaka kumsaidia mwenzao Enock Bella, katika masuala ya kimuziki ili kusudi aweze kuishi maisha mazuri kama walivyo wao.

Wa kwanza kulia ni Aslay, akifuatiwa na Enock Bella wa pili kutoka kulia na mwisho kushoto ni Beka Flavour.

Beka ametoa kauli hiyo alipokuwa anazungumza kwenye 'Backstage' ya BONGO FLAVA TOP20 kipindi kinachorushwa na East Africa Radio kila siku ya Jumamosi kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi 6:00 za mchana.

"Kuna vitu vitakuja hapo baadae kidogo, nimeona ni bora tufanye nyimbo japo moja 'special' kwa ajili ya kumsaidia Enock. Kwasababu mimi sitaki msanii yoyote wa Yamoto Band apate tabu kwenye maisha, nataka sote tuwe tunaishi vizuri kwenye maisha. Maana huwa naumia sana watu wanaponiambia mbona ndugu yako hafanyi vizuri", amesema Beka.

Aidha, Beka ameendelea kwa kusema kuwa "nashindwa kumuelewa mwenzetu Enock Bella ana kwama wapi ?, ila huwa tunawasiliana kila mara na anajitahidi kufanya 'collabo' na wasanii wengine lakini sijajua watanzania au mashabiki kwanini wanashindwa kumbeba ndugu yetu, naye akapata kusikika zaidi kama sisi wenzake".

Tokea lilipovunjika kundi la Yamoto Band miaka michache iliyopita, ilipelekea kila msanii aliyokuwepo katika kundi hilo, kufanya kazi kama 'solo artist', lakini kwa bahati mbaya hawakuweza wote kwa pamoja kupokelewa vizuri katika jamii licha ya awali walipokuwa kama kundi, walipendwa wote.

Enock Bella ni miongoni mwa wasanii waliokuwa wanavutiwa na wengi kipindi hicho, katika kundi la Yamoto Band kutokana na uzuri wa sauti yake ya 'base' lakini lilipokuja kuvunjika kundi hilo, ilimchukua muda mrefu hadi alipokuja kutoa kazi yake ya awali lakini hakuweza kupata mapokezi mazuri kwa kile walichokidai wadau wa muziki kuwa anauoga wa kufanya kazi ya pekee yake bila ya kundi kutokana na sauti yake.