Saturday , 4th May , 2019

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu, amesema kifo cha mwenyekiti mtendaji wa makampuni za IPP, Reginald Mengi kimeacha pigo kubwa wa wizara yake kutokana na mipango aliyokuwa nayo.

Kushoto ni Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akisalimiana na mtoto wa Dr. Mengi Abdiel Miku Mengi.

Ummy amesema hilo leo Mei 4, 2019, msibani nyumbani kwa marehemu Dr. Mengi Kinondoni Dar es Salaam ambako amefika kwaajili ya kutoa salamu za rambirambi kwa familia.

“Tumepoteza mtu muhimu alikuwa na mchango mkubwa kutokana na kuwa na dhamira ya dhati ya kuanzisha kiwanda cha dawa za binadamu hapa nchini, jambo ambalo tunawajibu wa kuliendeleza” amesema Ummy.

Waziri Ummy amesisitiza kuwa ni vigumu kuziba pengo lake lakini ameahidi atahakikisha kiwanda cha dawa alichokianzisha Dr. Mengi kinakamilika.

Waziri Ummy ndiye alizindua ujenzi wa kiwanda hicho katika eneo la Kerege, wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani, ambapo alieleza kuwa kukamilika kwa kiwanda hicho cha dawa za binadamu kutasadia kupunguza tatizo la ukosefu wa dawa nchini.