Sunday , 26th Aug , 2018

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, amewaagiza Maafisa uvuvi  kuweka hadharani tozo za samaki pamoja na mazao ya uvuvi kwa wafanyabiashara wa bidhaa hizo.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akizungumza na wafanyabiashara wa soko la samaki la kimataifa la  Kirumba jijini Mwanza.

Ulega ametoa agizo hilo leo katika soko la samaki la kimataifa la  Kirumba jijini Mwanza wakati wa ziara yake ya kutembelea miradi mbalimbali ya mifugo na uvuvi na kusema, masoko yote yaweke wazi tozo zote ambazo mfanyabiashara anatakiwa kulipa pindi anunuapo bidhaa.

Ulega ameeleza kuwa viongozi husika lazima wajue na kutambua majukumu yao bila kusubiri Waziri kuja kukagua maendeleo ya masoko na hivyo kuwataka maafisa na wafanyabiashara kukaa na kupanga mikakati ya kuongeza mapato ya Serikali ikiwa ni pamoja na Maafisa uvuvi  kutembelea masoko kila wiki ili kujua maendeleo yake.

Kuhusu udhibiti wa uvuvi haramu Ulega amewapongeza wavuvi kwa kutii sheria bila shuruti kwani hakuna nyavu haramu iliyokamatwa katika ukanda wa ziwa Viktoria na Kayenze.

Pia amewashauri wafanyabiashara kujua tozo wanazotakiwa kutoa kabla ya kununua mizigo kwani itawasaidia sana katika ufanyaji wao wa biashara kwa kutambua kiasi wanachotakiwa kulipa kama tozo kuliko kutoa tozo bila kujua nj kiasi gani wanatakiwa kulipa.

Mwezi  Februari mwaka huu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina kupitia oparesheni yake ya siku arobaini aliyoendesha katika mikoa ya kanda ya ziwa kupinga uvuvi haramu, alimwagiza katibu mkuu wa wizara hiyo anayeshughulikia uvuvi Dkt.Yohana Budeba pamoja na wakurugenzi wote wa halmashauri za wilaya katika mikoa ya kanda ya ziwa, kuwafuta kazi mara moja watumishi 65 na viongozi wa kamati za usimamizi wa raslimali za uvuvi (BMU) 26 baada ya kubainika wanashiriki kufadhili uvuvi haramu ndani ya ziwa Victoria.