Wednesday , 15th Apr , 2015

Wazee wastaafu wanaochukua pensheni zao kwenye mfuko wa hifadhi ya jamii wa PSPF wameulalamikia mfuko huo kwa kutowalipa fedha zao mpaka sasa.

Wazee mbalimbali wa chama na wastaafu wakiwa katika ukumbi huo ili wakimsikiliza Rais.

Wakizungumza na waandishi wa habari leo mjini hapa wazee hao wamesema kuwa kwa kawaida walitakiwa kupokea pensheni zao tangu April mosi mwaka huu lakini mpaka sasa hawajalipwa bila ya kuelezwa sababu zozote za msingi.

Akizungumza kwa niaba ya wazee hao, Ndijina Ndilito alisema kuwa tangu April mosi mwaka huu wamekuwa wakienda benki kuangalia kama fedha zao za pensheni lakini mpaka jana zilikuwa hazijaingia.

Alisema walipokwenda kwenye ofisi za PSPF mkoa wa Dodoma kuulizia kwa nini fedha zao hazijaingia mpaka muda huu waliambiwa kuwa fedha zao zimtumwa makao makuu ya benki ya NMB ambako wanachukulia fedha zao hivyo waendelee kusubiria mpaka hapo zitakapoingia.

Kwa upande wake ofisa wa PSPF Mkoa wa Dodoma, Rahim Hashim amesema kuwa yeye siyo msemaji wa mfuko huo na kwamba msemaji mkuu wa mfuko huo ni Mkurugenzi mkuu wa PSPF.

Hata hivyo Mkurugenzi mkuu wa PSPF Adamu Mayingu alipotafutwa kuzungumzia tuhuma hizo simu yake ya mkononi iliita bila kupokelewa.