Thursday , 30th Apr , 2015

Wakala wa Barabara Tanzania –TANROAD, imewafukuza kazi zaidi ya watumishi wake mia nne kutoka kitengo cha mizani zilizopo kwenye barabara kuu nchini kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo kuomba na kupokea rushwa.

Moja ya Miuzani za Tanroad katika barabara kuu nchini.

Waziri wa Ujenzi Dkt John Pombe Magufuli, amesema hayo jijini Dar es Salaam leo katika mkutano wake na baraza la wafanyakazi wa wizara ya ujenzi, mkutano ambao pia amewataka watendaji walio chini yake kutoogopa kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi wazembe na wala rushwa.

Kwa mujibu wa waziri Magufuli, hatua hiyo itaongeza ufanisi katika utendaji wao ambapo ametolea mfano jinsi hatua ya Tanroad ilivyopandisha rekodi ya utendaji wa taasisi hiyo kiasi cha kuibuka kuwa ya tatu barani Afrika baina ya wakala zenye jukumu la usimamizi wa miundombinu ya barabara kwa mujibu wa ripoti ya benki ya dunia.

Akizungumzia mafanikio hayo ya TANROAD, waziri Magufuli amesema nafasi ya wakala wa kwanza imeshikwa na Afrika Kusini, kifuatiwa na ile ya nchini Botswana wakati TANROAD imeshika nafasi ya tatu.