Wednesday , 11th May , 2016

Wakazi wa kijiji cha Nahama Kata ya Namayuni wilayani Kilwa mkoani Lindi, wanalazimika kutembea umbali wa Kilometa 25 hadi 32 kufuata huduma za afya, hali inayopelekea baadhi ya wajawazito kujifungulia nyumbani mwao, njiani na wengine kupoteza maisha

Mkurugenzi wa Wilaya ya Kilwa Twalib(Kulia) Mbasha akikabidhiwa kataba wa miradi ya ujenzi wa nyumba

Wakizungumza na East Africa Radio, wamesema kutokana na kukosa huduma hizo kijijini hapo, mwaka 2010 walianza ujenzi wa Zahanati kupitia nguvu zao wenyewe ambapo mwaka 2014 serikali ya halmashauri ya wilaya ya Kilwa ikaweka jiwe la msingi na kuahidi kukamilisha ujenzi huo ambao hadi sasa hakuna kilichofanyika.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Twalibu Mmbasha, amekiri uwapo wa changamoto hiyo ambapo amesema suala linalokwamisha ni ukosefu wa fedha za mapato ya ndani ambazo zinategemewa pia kutatua changamoto katika sekta za elimu, maji na miundombinu.

Aidha, Mkurugenzi huyo amewataka wananchi hao waendelee kujitolea kuchangia katika miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo hayo ili kutatua changamoto hizo zinazowakabili katika kupata huduma muhimu za kijamii.