Sunday , 10th Jan , 2016

Mkoa wa Arusha umepiga marufuku watu wenye tabia ya kutapisha vyoo kiholela,ikiwa ni sehemu ya kukabiliana ugonjwa wa kipindupindu na kuahidi hatua kali za kisheria dhidi yao, pamoja na wale wanaoishi bila vyoo.

Mkuu wa Mkoa Arusha Daudi Felix Ntibenda

Wakazi wa Arusha wakizungumzia hatua hiyo wamesema kuwa kuzagaa kwa vinyesi hususan katika maeneo yenye upungufu wa vyoo na uhaba wa maji kumekuwa kukichochea magonjwa ya mlipuko hivyo wananchi hawana budi kutilia mkazo suala la matumizi ya vyoo.

Antony Ashery ni mkazi wa Morombo Arusha amesema kuwa ugonjwa huo unatokana na uchafu ili kuondokana na ugonjwa huo wakazi wa Arusha wanapaswa kujenga utamaduni wa kuwa wasafi.

Mkazi wa Ngaramtoni Aron Peter amesema kuwa ili kutokomeza ugonjwa huo serikali inatakiwa kusimamia sheria za mazingira na kushirikiana na wananchi ili kudhibiti uchafu unasababisha kipindupindu

Hata hivyo Mkuu wa Mkoa Arusha Daudi Felix Ntibenda katika mkutano wake na viongozi wa serikali na taasisi binafsi juu ya ugonjwa wa kipindupindu ametoa karipio kwa wananchi wanaotapisha vyoo kwani serikali haitawafumbia macho na pia ameagiza minada yote isiyo na vyoo ifungwe mpaka pale ujenzi wa vyoo utakapokamilika.