Monday , 29th Sep , 2014

Watanzania wametakiwa kuchukua tahadhari kwa kutojihusisha na matendo hatarishi ambayo huchochea kukuza hatari za kupata ugonjwa wa Moyo ambapo magonjwa hayo husababisha vifo kwa takribani watu milioni 17.3 duniani kila mwaka.

Nyama pamoja na vyakula vyenye kiwango kikubwa cha mafuta ni moja ya chanzo cha ugonjwa wa moyo.

Akiongea leo jijini Dar es salaam, Daktari bingwa wa magonjwa ya Moyo wa Hospitali ya taifa ya Muhimbili Dkt. Delilah Kimambo amesema ili kupunguza athari za kupata ugonjwa wa moyo, watu kula chakula bora,kufanya mazoezi na kuacha kuvuta sigara,.

Dk Kimambo amesema siku ya afya ya moyo duniani ilianza ikiadhimishwa kutokana na magonjwa ya moyo kusambaa na kuongoza kwa vifo duniani na kuongeza kuwa ikiwa elimu ya uelewa kuhusu ugonjwa wa moyo itatolewa ipasavyo utapunguza idadi ya vifo vitokanavyo na ugonjwa huo.

Wakati huo huo, Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi nchini Tanzania (NACTE) limesema wanafunzi wengi wa stashahada wanaoomba kujiunga na vyuo vya elimu ya juu ili kuendelea katika ngazi ya shahada kupitia Baraza hilo wanakosa nafasi kutokana na uchache wa nafasi zilizotengwa na serikali katika vyuo hivyo.

Akiongea na East Africa Radio leo jijini Dar es salaam, Katibu Mkuu wa NACTE, Dkt. Primus Nkwera amesema serikali imetoa kipaumbele kwa wanafunzi wengi wanaohitimu kidato cha sita hali inayoiathiri idadi kubwa ya wanafunzi wenye stashahada wanaohitaji kuendelea na shahada katika vyuo vya elimu ya juu nchini.

Dkt. Nkwera amesema kwa mwaka huu NACTE imepokea jumla ya maombi ya wanafunzi elfu kumi na sita wenye stashahada na waliopata nafasi za kujiunga na vyuo hivyo ni elfu tisa pekee huku idadi ya wanafunzi wa kozi za Afya waliokosa nafasi ya kuendelea katika vyuo vya elimu ya juu wakiwa ni wengi zaidi kutokana na ufinyu wa nafasi hizo.