Wednesday , 30th Dec , 2015

Baadhi ya wanawake wa kijiji Mpinga kilichopo wilayani Bahi, mkoani Dodoma wamelalamika kutelekezwa na wanaume zao kutokana na tatizo la njaa linalokikabili kijiji hicho.

Mbunge wa Jimbo la Bahi, Omar Badwel, akisalimiana na wananchi wa Kijiji cha Kigwe, Wilaya ya Bahi

Wakizungumza na East Africa Radio wanawake hao wamesema kuwa kufuatia kijiji hicho kukabiliwa na njaa baadhi ya wanaume zao wameamua kuhama nyumbani kwa madai ya kwenda kutafuta vibarua lakini hawajawahi kurudi kwenye familia zao mpaka sasa.

Tiliza Lebanyi amesema kuwa imekuwa ni tabia ya wanaume wa kijiji hicho kutoroka kipindi cha njaa kwa madai ya kwenda kutafuta vibarua lakini huwa hawarudi mpaka njaa inapoisha.

“Hivi unavyoniona mume wangu haonekani tangu mwezi wa kumi na moja na aliniaga kuwa anakwenda kutafuta vibarua hajarudi hadi leo na ameniacha na watoto wadogo ambao peke yangu siwezi kuwalisha,” alisema Tibanyi na kuongeza kuwa,

“Naiomba serikali kama ina chakula cha msaada watusaidie ili waume zetu warudi nyumbani tusaidiane kulima mashamba kwa kuwa hiki ni kipindi cha msimu wa kilimo.”

Naye Martha Mtangoo amesema kuwa katika kipindi cha njaa wanawake wengi huwa wanapata shida ya kulea familia peke yao bila msaada wa waume zao hali inayowafanya kushindwa kutekeleza majukumu mengine hasa ya kilimo.
Amesema kuwa wamekuwa wakikimbiwa na waume zao kwa muda mrefu hali ambayo huwawia vigumu kulea familia zao ambazo ambazo ni kubwa.

Magdalena Matonya amesema kuwa kutokana na hali iliyopo ya njaa wanalazimika kufanya kazi ya vibarua vya kuuza maji katika machimbo yaliyopo kijijini hapo kwa ujira mdogo ambao wanaoupata lakini hata hivyo haukidhi mahitaji.

“Tunalazimika kuuza maji kwa ndoo moja shilingi 300 ambapo kwa siku unaweza kufanikisha kuuza ndoo mbili hadi tatu na fedha tunayoipata tunanunua unga kibaba kimoja ambacho tunakitumia kukoroga uji au mlo wa siku moja tu,” alisema Matonya
Amesema kutokana na hali hiyo hawana pakukimbilia hivyo wameiomba serikali iwasaidie uwezekano wa kupata chakula cha bei nafuu.

Naye diwani wa kata hiyo ya Mpinga Gaitani Muyinga amekiri kuwepo kwa tatizo hilo la njaa kwa wananchi wake, alisema kuwa amekuwa akipokea malalamiko kutoka kwa wanawake kutelekezwa na waume zao huku wakimuomba msaada.
Hata hivyo amesema kuwa kitendo cha wanaume hao kutelekeza familia zao kwani kijiji kinabaki hakina wanaume ambao kama tatizo kubwa linalohitaji nguvu kazi litatokea wanawake watashindwa kulitatua.

Muyinga ameiomba serikali kupitia ofisi ya mkuu wa wilaya kitengo cha maafa kuharakisha msaada wa chakula kutokana na wananchi wake kuwa katika hali mbaya suala ambalo linaweza kuhadhiri hata mahudhuria ya watoto mashuleni.