
Pichani ni bei za nafaka, sokoni.
Wakizungumza na eatv.tv baadhi ya wafanyabiashara akiwemo Mama lishe, Amina Hussein amesema kuwa mfumuko wa bei kupungua wao kama wafanyabishara wa vyakula hawaoni tofauti inayopelekea takwimu hizo kushuka.
“Sielewi hilo suala la kushuka kwa bidhaa, kila siku bidhaa zinaongezeka bei mafuta ya kula, sukari na matunda, hapo awali chai ya rangi tulikuwa tunauza sh. 100 lakini sasa hivi ni sh. 300”, amesema Mama Lishe.
Naye mmoja kati ya wateja wa chakula Catherine Paul amefunguka kuwa bei za vyakula kwa mama lishe zimeongezeka na kupelekea kuhamia kwenye vibanda vya chipsi ili kuendana na hali halisi ya vipato vyao.
“Nafanya kazi kiwandani mfano nalipwa shilingi elfu nne kwa siku, siwezi lipa chakula elfu mbili. Nitaishi vipi sasa nitajikaza tu nikanunue hata chipsi za sh. 1000”, amesema.
Kwa upande wao wadau wa usafirishaji, akiwemo Bakari Hemed amesema kuwa ongezeko la mafuta kwa sasa halijatazama ongezeko la nauli pia hivyo kupelekea changamoto baina yao na wateja maana wanapoongeza bei huibua migogoro na wateja kutokana na hali halisi ya maisha ya sasa.
“Mafuta yamepanda, na mafuta yakipanda bei kila kitu kinapanda sasa hizi takwimu za kushuka kwa mfumuko wa bei hatujaelewa ni za muda upi maana mambo ni tofauti mafuta yamepanda lakini nauli ziko palepale”, amesema Hemed.
Mfumuko wa bei kwa kipindi cha mwaka unaoishia mwezi Juni mwaka huu umeendelea kushuka kutoka asilimia 3.6 ilivyokuwa mwezi Mei hadi asilimia 3.4, huku sababu kuu iliyochangia kushuka huko ikiwa ni kupungua kwa kasi ya bidhaa zisizo za vyakula.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu jana imetangaza kushuka kwa mfumuko wa bei nchini ambapo zilionesha hali ni tofauti kidogo kwa nchi za Kenya na Uganda ambako mfumuko wa bei umepanda kiasi.