Thursday , 19th May , 2016

Baadhi ya wananchi wa Tarafa ya Mikindani mkoani Mtwara, wamewalalamikia madiwani wao kutoka vyama mbalimbali vya kisiasa kutokana na kutokuwa na umoja na nia ya kuwaletea maendeleo wananchi.

Mkuu wa mkoa wa Mtwara Halima Dendego akizungumza na watumishi wa Halmashauri.

Akizungumza mbele ya Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, alipofanya kikao cha kazi na wakazi wa kata ya Jangwani katika tarafa hiyo, Ahmad Mkumilwa, amewaita madiwani hao kuwa ni wanafiki na kwamba kama hawataki kuwatumikia wananchi wao waliowachagua wajiuzulu.

Mwananchi huyo amemadai kuwa madiwani hao hawana utaratibu wa kukutana kupanga mipango ya maendeleo kwa pamoja na badala yake wamekua wakifanya ushindani wa kisiasa na kuwasahau wananchi.

Katika hatua hatua nyingine, Mkumilwa, amekemea tabia za baadhi ya wakazi wenzake wa mji wa Mikindani kutopenda kuwa na vyoo na kuamua kujisaidia katika nyumba za watu wacheche walionavyo au katika fukwe za bahari, na kuwataka wenyeviti kukemea vikali tabia hiyo.

Mkuu wa mkoa, amemwagiza afisa tarafa ya Mikindani, Francis Mkuti, kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja kila nyumba inakuwa na choo, ambapo aliahidi kurudi baada ya muda huo kukamilika kwa ajili ya kukagua utekelezwaji wa agizo lake.