Mratibu wa Chama cha Utabibu wa Tiba Asili nchini Tanzania - ATME, Boniventura Mwalongo.
Mratibu wa chama cha watabibu wa tiba asili nchini Tanzania Bw. Boniventura Mwalongo, amesema hayo leo jijini Dar es Salaam na kufafanua kuwa ukosefu wa taarifa na elimu ya kutosha umeifanya jamii ishindwe kutofautisha kati ya tiba asili na matendo ya kiovu yanayofanywa kupitia kivuli cha tiba asili.
Mwalongo amesema kuwa kwa kutumia taaluma na weledi wao, waandishi wa habari nchini wanaweza kuisadia jamii kwa kuifahamisha juu ya umuhimu wa tiba asili na hivyo kuinusuru dhidi ya adha wanayoipata kutoka kwa waganga wa kienyeji ambao wamekuwa wakiwafanyia matendo ya kinyama ikiwa ni pamoja na kuwabaka na kuwarubuni kiasi kikubwa cha pesa.
Wakati huo huo, Shirikisho la vyama vya wafanyakazi nchini Tanzania (TUCTA) limesema hali ya wafanyakazi haswa wa sekta binafsi nchini bado ni mbaya kimazingira na maslahi sambamba na waajiri kupuuzia haki za wafanyakazi.
Katibu Mkuu wa TUCTA Bw. Nicholaus Mgaya ametoa kauli hiyo leo wakati akielezea hali ya wafanyakazi hapa nchini na muitikio wa waajiri kuboresha mazingira ya wafanyakazi.
Bw. Mgaya amesema kukua kwa tatizo la waajiri kupuuzia wafanyakazi na wafanyakazi kukosa stahiki zao kunatokana na wafanyakazi wenyewe kutosoma sheria na kushindwa kufahamu haki zao.