Monday , 23rd May , 2016

Wagonjwa wanaokwenda kutibiwa katika kituo cha afya cha Kitere halmashauri ya wilaya ya Mtwara wanashindwa kupata huduma za upasuaji kutokana na kituo hicho kukabiliwa na uhaba wa watalaamu wa huduma hizo.

Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego.

Mganga Mkuu wa kituo hicho, Dkt. Dickson Hokololo, amemweleza changamoto hizo Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, ambaye alifika kituoni hapo kukagua utendaji kazi na kusikiliza changamoto zilizopo ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika halmashauri hiyo.

Mkuu wa Mkoa huyo ametoa siku 20 kwa uongozi wa kituo hicho kuhakikisha kinaanza kutoa huduma hizo na kuwaondolea usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kina mama wajawazito kufuata huduma za upasuaji katika hospitali ya rufaa ya Ligula mjini Mtwara.

Aidha, Dendego amesisitiza juu ya uhamasishaji wa wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ambao utasaidia wananchi kupata matibabu bure na kituo kujiendesha chenyewe iwapo watu watajiunga kwa wingi.

Kituo cha afya cha Kitere ni tegemeo kwa wananchi wote wa kata hiyo na vijiji jirani ambapo chumba cha upasuaji kimekamilika na kina vifaa vyote vinavyohitajika isipokuwa huduma zinashindikana kutolewa kutokana na kukosa wataalamu.