Wednesday , 1st Apr , 2015

Wananchi wa kijiji cha Itengelo kata ya Saja wamegoma kuendelea kuandikishwa katika daftari la kudumu la mpigakura kwa mfumo wa kielektroniki (BVR) kufuatia uongozi wa kijiji hicho kuwahamishia katika kata mpya ya Uhenga badala ya kata ya zamani Saja

Ofisa uandikishaji katika Daftari la Kudumu la Wapiga kura, Alen Simon (kulia) akichukua taarifa muhimu za wakazi wa Mangula, Makambako waliojitokeza

Mgomo huo umetokea jana katika kata hiyo ambapo wananchi hao wametakiwa kujiandikisha katika kata ya Saja na kutakiwa kuhamishiwa katika kata ya Uhenga ambako serikali ya kijiji hicho ilitaka wahamie huko.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi wa kijiji cha Uhenga wamesema wanapinga kupelekwa katika kata ya Uhenga badala yake wabaki katika kata ya Saja kwa kuwa kata ya Uhenga iko mbali na imewapelekea kushindwa kupata huduma ikilinganishwa na Saja walikozoea.

Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Gaston Mlimbila alilamikia kitendo cha wananchi kushindwa kushirikishwa wakati wa uanzishwaji wa kata mpya lakini katika hali ya kushangaza wananchi hao hawakushirikishwa jambo ambalo wao hawako tayari kujiandikisha kwenye kata ambayo wao hawaitambui.

Diwani wa Kata ya Saja Andrew Mangula pamoja na kuwasihi wananchi kwenda kujiandikisha juhudi zake zimegonga mwamba baada ya wananchi kushikilia msimamo wa kugomea kwenda kujiandikisha kwa madai kuwa hawataki kujihalalisha kuwa wakazi wa kata ya Uhenga.

Amewataka wanakijiji hao kuanza mchakato wake huo sasa, lakini suala hilo linabidi lipitie hatua mbalimbali hadi kukamilika, ikiwa ni pamoja na kujadiliwa na Baraza la Maendeleo la Kata (BMK), Kikao cha Baraza la Madiwani na hatimaye kwenda kwenye kikao cha ushauri cha maendeleo ya wilaya (DCC) na kile cha mkoa (RCC) na kisha kwenda Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa ajili ya kupitishwa..

Hata hivyo diwani Mangula amemtupia lawama mwenyekiti wa zamani wa kijiji hicho Henry Ngajule kwa kushindwa kutoa mrejesho kwa wananchi wake baada ya maazimio yaliyokuwa yakijadiliwa kwenye BMK.

Alipotafutwa kutolea ufafanuzi juu ya uamuzi wa wananchi wa kata ya Uhenga kugomea kujiandikisha, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe Emmanuel Kilundo kwa njia ya simu amesema kwamba atalitolea ufafanuzi suala hilo baada ya kupata taarifa juu ya suala hilo.
….................................................