Thursday , 7th Apr , 2016

Baadhi ya wachumi nchini Tanzania wamepongeza bajeti pendekezwa ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha kwa maelezo kuwa bajeti ya mwaka huu imezingatia haja ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi.

Walioipongeza bajeti hiyo ni pamoja na Mchumi na mtafiti mwandamizi kutoka asasi ya REPOA Dkt. Abel Kinyondo, ambaye amesema hatua ya kutenga asilimia arobaini ya fedha kwenda kwenye shughuli za maendeleo inaonyesha nia ya serikali ya awamu ya tano ya kukabiliana na umaskini na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Kwa mujibu wa Dkt Kinyondo, moja ya maeneo ambayo ni mazuri ni pamoja na mapendekezo ya kuongeza kiwango cha pesa zinazoelekezwa kwenye miradi ya maendeleo tofauti na miaka iliyopita ambapo pesa zinazotengwa kwa ajili ya uendeshaji wa serikali ndio zilikuwa zinachukua sehemu kubwa ya bajeti.

“Tumeona katika bajeti ijayo kiasi cha pesa kitakachokwenda kwenye shughuli za maendeleo ni takribani asilimia arobaini...hii ni ishara nzuri kwamba serikali ya awamu ya tano imejipanga kupunguza umaskini na kuharakisha maendeleo, alisema Dkt Kinyondo.

Aidha, Dkt Kinyondo ameongeza kuwa hata vipaumbele vya bejeti hiyo vinaakisi mipango ya kiuchumi iliyonayo serikali hivi sasa, ikiwa ni pamoja na kupunguza utegemezi wa wahisani katika bajeti ambao umeshuka na kufikia asilimia kumi na mbili.

“Bajeti hii inaendana na mipango ya sasa ya maendeleo kupitia dhana ya uchumi wa viwanda na kitu kizuri ni kwamba hata utegemezi wa wahisani katika bajeti nao umepungua na kufikia asilimia kumi na mbili,” alisema Dkt Kinyondo