Friday , 8th Dec , 2017

Wafanyabiashara zaidi ya 550 waliovunjiwa vibanda vyao na kampuni hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO) mjini Dodoma wanatarajiwa kupatiwa eneo kwaajili ya kuwawezesha kuendelea kufanya biashara zao kama kawaida.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi, alipotembelea eneo la Jamatini na Stendi Kuu Novemba 6 mwaka huu, akiambatana na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Vijana na Ajira Anthony Mavunde.

Mkurugenzi amewapa pole wafanyabiashara hao na kuwapa moyo kuwa shughuli zao zitaendelea kama kawaida baada ya taratibu za kupewa eneo jipya kukamilika.

“Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge ametoa maelekezo kwa Manispaa na Sumatra kuhakikisha daladala zinakuwa na ruti inayopita katika eneo hilo jipya la biashara ambapo abiria watakuwa na kituo cha kupanda na kushuka na hivyo kuongeza mzunguko wa wateja katika eneo hilo, na utekelezaji wa maelekezo hayo umeshaanza kufanyiwa kazi na Sumatra”, amesema Kunambi.

Naye Naibu Waziri Mavunde  ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma, amewataka wote walioathiriwa na zoezi hilo la bomoabomoa wawe watulivu katika kipindi hiki kigumu wakati Mamlaka na viongozi wakifanya juhudi za makusudi kuwatafutia maeneo rafiki kwa shughuli zao.

Wafanya biashara hao walivunjiwa vibanda vyao katika kituo cha mabasi madogo cha  Jamatini ili kupisha utekelezaji wa mradi wa Reli ya kisasa.