Monday , 30th May , 2016

Ukosefu wa ajira na hali mbaya ya kiuchumi inayowakabili vijana nchini itapungua iwapo vijana hao watajiunga na vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi (VETA) ambayo sasa vinatoa mafunzo yanayoweza kuwapatia vijana ujuzi wa kujiajiri na kuajiriwa.

Meneja Uhusiano wa Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini VETA, Bw. Sitta Peter.

Meneja Uhusiano wa Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini (VETA), Bw. Sitta Peter, amesema hayo katika mahojiano na Hotmix na kutaja fani ambazo zina fursa ya ajira na kiuchumi kwa wahitimu wake kuwa ni za ufundi, huduma katika sekta ya mafuta na gesi pamoja na ujuzi wa kuanzisha miradi na biashara ndogo ndogo.

"Mafunzo tunayoyatoa yana umuhimu mkubwa kwa uchumi wa nchi, tunatoa mafunzo kwa ajili ya kujiajiri au kuajiriwa na sekta binafsi na hata kwenye taasisi za umma," amesema Sitta.

Sitta amesema VETA wanatoa mafunzo ya yanayoendana na mahitaji ya uanzishaji wa viwanda vidogo na kwamba hiyo ni fursa ya vijana kujipanga ili kuwa sehemu ya kundi la watu watakaofaidika na mpango wa serikali ya awamu ya tano ya kuwa na Tanzania ya viwanda.

Aidha, Sitta amefafanua hoja kuhusu mafunzo ya VETA katika fani ya mafuta na gesi na fursa ya kiuchumi kwa wahitimu wa fani hiyo mpya hapa nchini ambapo amesema tofauti na inavodhaniwa na wengi, mafunzo yanayotolewa na VETA ni kuwapa vijana wa Kitanzania ujuzi na fani zitakazowawezesha kuajiriwa kama mafundi mchundo huku wengine wakitoa huduma zinazohitajika katika miradi ya utafutaji wa mafuta na gesi.