Vyama vya Siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi nchini Tanzania (UKAWA) leo vimetangaza rasmi kuwa vitasusia kushiriki kura ya maoni, zoezi ambalo ni hatua muhimu katika mchakato wa kupata Katiba mpya na ambalo litafanyika April 30 mwaka huu.
Viongozi wakuu wa vyama vinavyounda UKAWA wametangaza uamuzi huo leo jijini Dar es Salaam , ambapo Mwenyekiti Mwenza wa UKAWA Profesa Ibrahim Lipumba ameelezea sababu za wao kutoshiriki na namna watakavyoshawishi wananchi nao wasishiriki zoezi hilo.
Ameelezea sababu kubwa ya kususia zoezi hilo kuwa ni kwamba mchakato wa kuipata Katiba Inayopendekezwa haukuwa halali, na hivyo Katiba Inayopendekezwa si halali na hivyo hawawezi kushiriki katika kitu haramu..
Lipumba amesema kuwa maandalizi ya kuandisha wapiga kura hayaridhishi, na kwamba vifaa vya BVR vilivyopo nchini hadi sasa ni 250, makubaliano ya tume ilikuwa ni kuwa na vifaa 15,000, lakini serikali ilikubali kugharamia vifaa 8000, na kwa mujibuwa NEC vituo vya kupigia kura vinatarajia kuwa 40,015 kwahiyo ni ndoto kuwaandikisha wapiga kura milioni 23 hadi kufikia April 30.
Sababu nyingine iliyotajwa ni kwamba wananchi bado hawajaielewa Katiba Inayopendekezwa, na serikali haifanyi juhudi zozote kuchapisha nakala za katiba hiyo ili wananchi waielewe.
Emanuel Makaidi amesema “Haramu haiwezi kuzaa halali, ingawa halali inaweza kuzaa haramu,…” kwahiyo wao walisusia mchakato ambao ulikuwa haramu, hawawezi kuunga mkono zao la mchakato haramu.
Freeman Mbowe “Tumejitoa na hatutarudi kwa gharama yoyote, BVR watu hawajui na hakuna maandalizi yoyote…… CCM wanataka kuliingiza taifa kwenye machafuko.
Wenyeviti hao wamesema kuwa kama serikali italazimisha mchakato huo, basi itegemee vituo vya kupigia kura siku hiyo kutokuwa na watu kabisa, hali ambayo huenda ikasababisha machafuko.
Wakati UKAWA wakitangaza kususia Kura ya Maoni, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) nacho kimeitaka serikali kusitisha zoezi hilo kwa madai ya mapungufu kadhaa ikiwemo maandalizi hafifu, pamoja na mapungufu katika sheria ya kura ya maoni.
Mkurugenzi Mkuu wa kituo hicho Bi. Hellen Kijo-Bisimba amesema kuwa udhaifu huo wote unalenga kulinufaisha kundi fulani la watu katika jamii.