Thursday , 16th Oct , 2014

Viongozi wa juu wa vyama vinayounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA, wanakutana jijini Dar es Salaam jioni hii kujadili kile walichokiita kuwa ni mpango wa kudumu wa kuunganisha nguvu kwa ajili ya kushinda uchaguzi mkuu wa mwakani.

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Dkt Wilbrod Slaa.

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Dkt Wilbrod Slaa, amesema hayo jijini Dar es Salaam leo wakati akitoa maazimio ya Kikao Maalum cha Kamati Kuu ya chama hicho, iliyokutana jijini Dar es Salaam kujadili masuala mbali mbali ukiwemo mchakato wa katiba mpya pamoja na chaguzi zinazotarajiwa kufanyika kati ya sasa na mwakani.

Kwa mujibu wa Dkt Slaa, ushirikiano unaoratibiwa chini ya UKAWA, unakwenda mbali zaidi ya mchakato wa katiba mpya na kwamba jukumu kuu lililo mbele yao hivi sasa ni kuhakikisha wanaunganisha nguvu kushinda chaguzi hizo, hatua aliyosema itasaidia kukiondoa madarakani chama tawala CCM.

Aidha, muungano wa asasi za kiraia katika masuala ya jinsia na Katiba nchini Tanzania umewashauri wananchi kuisoma na kuilewa katiba pendekezi kabla ya kutoa maoni yao ili kuwa na ufahamu wa kutosha wa kile kichomo ndani ya katiba hiyo.

Mwenyekiti wa muungano huo Bi. Victoria Mandari ametoa ushauri huo jijini Dar es salaam ikiwa ni tamko la pamoja la muungano huo unaounda mashirika kadhaa yasiyo ya kiserikali hapa nchini.

Amesema kumekuwepo na shinikizo la kisiasa la kuwataka watanzania waikatae katiba hiyo pendekezi jambo ambalo linaweza kusababisha hata yale mazuri yaliyokuwepo ndani ya katiba hiyo yakaonekana ni mabaya.