Wednesday , 17th Feb , 2016

Serikali ya Ujerumani imeipa Tanzania msaada wa ndege mbili kwa ajili ya kufanya doria za angani katika hifadhi ya Serengeti na pori la akiba la Selous ili kudhibiti uwindaji haramu na kukabiliana na majangili.

Waziri wa Maliasili na Utalii Profesa, Jumanne Maghembe.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya msaada huo Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe amesema zaidi ya ndege hizo serikali ya Ujerumani pia imeisaidia Tanzania shilingi bilioni 80 kwa ajili ya masuala ya uhifadhi katika kipindi cha miaka mitano ijayo ikiwemo kuanzishwa kwa Mamlaka ya Ulizi wa Wanyamapori(TAWA).

Kwa upande wake balozi wa Ujerumani hapa nchini Egon Konchake amesema nchi yake imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa masuala ya uhifadhi duniani yanatiliwa umuhimu na kwamba zaidi ya dola za Marekani milioni 300 zimewekwa kwa ajili ya shughuli hiyo pekee.

Ndege hizo mbili zina thamani ya shilingi milioni 1.2 na tayari zimeanza kazi na watu wanne watuhumiwa wa ujangili wamekamatwa kwa mujibu wa Mhifadhi Mkuu wa Serengeti, Wiliam Mwakilema.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa Dkt. Allan Kijazi ameishukuru serikali ya Ujerumani na kwa ndege hizo na kusema kuwa ilikuwa vigumu kufanya doria katika eneo la Serengeti lenye ukubwa wa Kilometa za mraba 14,700 kwa kutumia magari au askari wa miguu pekee.