Thursday , 9th Oct , 2014

Tatizo la wanafunzi wa kike kukatisha masomo kutokana na kupata ujauzito katika wilaya ya kilolo

Katibu Mkuu wa CCM akiwa ziarani mkoani Iringa

Tatizo la wanafunzi wa kike kukatisha masomo kutokana na kupata ujauzito katika wilaya ya kilolo mkoani Iringa bado ni kubwa ambapo zaidi ya wasichana 12 wa sekondari wameshindwa kumaliza masomo yao kwa kipindi cha mwaka jana peke yake.

Hayo yamebainishwa na mkuu wa wilaya ya kilolo Bw Gerald Guninita kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Utengule alipokuwa akijibu baadhi ya kero za wananchi walizokuwa wakimweleza katibu mkuu wa CCM Bw Abdulrahman Kinana ambapo amekiri tatizo hilo kuwa linaisumbua wilaya yake na kuongeza kuwa katika kupambana nalo wametunga sheria ndogondogo za halmashari na tayari wameshazipeleka kwa waziri mkuu.

Baadhi ya wananchi waliopata nafasi ya kuuliza maswali pamoja na mambo mengine wameeleza kusikitishwa na kitendo cha serikali kushindwa kuwachukulia hatua watu wanaohusika na kuwapa mimba wanafunzi hali inayochangia tatizo hilo kuongezeka kila siku na baadhi ya walimu wakielezea mazingira magumu wanayofanyia kazi ikiwemo shule kuwa na vyumba viwili tu vya madarasa ilihali wana wanafunzi kuanzia chekechea hadi darasa la Sita.

Katibu mkuu wa CCM Bw Abdulrahiman Kinana mbali na kueleza mikakati ya serikali inayoongozwa na chama chake amesema kwa sasa shule za sekondari za kata zimepiga hatua tofauti na awali na kwamba mchakato unaoendelea wa kujenga maabara shule zote nchini utainua kiwango cha elimu kwa kiasi kikubwa, huku katibu wa itikadi na uenezi wa chama hicho Nape Nnauye akieleza mikakati kadhaa waliyonayo kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Desemba mwaka huu.