Naibu Kamishna na Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji nchini Tanzania, Abbas Mussa Irovya.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Naibu Kamishna na Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji nchini Tanzania Bw. Abbas Irovya amesema taarifa hizo ni za uzushi zilizotumia baadhi ya matukio ya ukweli katika kupotosha jamii.
Irovya ametaja baadhi ya matukio hayo kuwa ni maamuzi ya kumfukuza nchini raia mmoja wa kigeni ambaye alikuwa akijihusisha na biashara haramu ya kusafirisha binadamu.
Katika hali ya kushangaza, Bw. Irovya amesema chombo hicho cha habari imezichukua taarifa hizo na kuzibadilisha kwa kuwaeleza wananchi kwamba raia huyo wa kigeni amerejea nchini na yupo jijini Arusha kwa msaada wa viongozi waandamizi wa Idara hiyo.
Matukio mengine ni pamoja na yale ya kuingia nchini kwa raia wa kigeni na kwamba mwandishi wa habari hiyo amediriki hata kutaja namna wahamiaji hao haramu wanavyoingia nchini kwa kile ambacho mwandishi huyo anadai kuwa ni njama zinazoratibiwa na kigogo mmoja wa idara ya Uhamiaji ambaye ana mpango wa kugombea ubunge na hata ateuliwe kuwa waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Naibu Kamishna Irovya amewataka wananchi kupuuza habari hizo za kupikwa zenye lengo la kuchafua utendaji wa idara ya uhamiaji na kwamba maofisa wa idara hiyo wanafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kuwa wahamiaji haramu hawaingii nchini.
Aidha, katika hatua nyingine, Naibu Kamishna Irovya amesema idara yake imeanza kutekeleza maboresho ya namna inavyopata taarifa za watu wanaoingia nchini kupitia mfumo wa kisasa ujulikanao kama Advanced Passengers Information System au kwa kifupi kama APIS.
Irovya amefafanua kuwa mfumo huo unasaidia kupatikana haraka kwa taarifa muhimu za wageni wote wanaoingia nchini kwa kutumia viwanja vya ndege na mipaka, hatua itakayowasaidia kubaini uhalali wa wageni hao kuwa nchini pamoja na mienendo na mambo mengine yanayoweza kuhatarisha amani.