Thursday , 28th Jul , 2016

Timu ya wataalam wa tiba kutoka nchini China wanaokuja nchini Tanzania kusaidia kutoa huduma za tiba katika hosipitali ya taifa ya muhimbili wamesema kuwa wamevutiwa sana kufanya kazi nchini Tanzania.

Baadhi ya wataalam wa tiba kutoka nchini China

Wamesema sababu zinazowafanya kuvutiwa ni kutokana na ukarimu walioupata katika kipindi chote cha miaka kumi walizoshiriki kufanya kazi nchini Tanzania.

Mtafsiri na msemaji wa timu hiyo Bw. Song Tao ambaye kwa sasa anamaliza muda wake pamoja na madaktari wengine wa timu ya wataalam wa tiba wa China wamesema kuwa kutokana na ukarimu walioushuhudia katika miaka kumi ya uwepo wao nchini Tanzania, wangependa kuendelea kuwepo nchini hata kwa kazi nyingine yoyote.

Tao ameeleza kuwa wachina wengi wanaofika hapa nchini wamekuwa wakitamani zaidi kuendelea kufanya kazi Tanzania hata mara baada ya kuisha kwa muda wa kazi maalum walizopangiwa kuja kufanya kazi hapa nchini.

Kwa mara ya kwanza serikali ya China ilianza kuwatuma wataalam wake wa kutoa tiba hapa nchini mnamo mwaka 1968 na wataalam hao wameendelea kufurahia historia nzuri ya ukarimu uliokuwepo tangu kuanza kwa zoezi hilo baina ya serikali ya Tanzania na China.

Wataalam hao wa tiba wanaondoka nchini Tanzania mapema mwezi huu huku wakifungua milango kwa serikali ya Tanzania na China kuwapa tena nafasi ya kuwepo Tanzania ikiwezekana.