Friday , 11th Apr , 2014

Mamlaka ya hali ya hewa nchini Tanzania TMA imetoa tahadhari juu ya kuwepo kwa mvua kubwa kuanzia leo mpaka tarehe 14 ya mwezi huu itakayozidi kiwango cha wastani wa asilimia 70.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TMA, hali hiyo inatokana na kuimarika zaidi kwa ukanda wa mvua ambao umeambatana na ongezeko la unyevunyevu katika eneo la bahari ya Hindi.

Maeneo ambayo yataathirika zaidi na mvua hizo ni pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba, mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, na pia kuna uwezekano wa kusambaa katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Morogoro.

TMA imetoa tahadhari kwa wakazi wa maeneo hatarishi, watumiaji wa Bahari pamoja na mamlaka zinazohusika na maafa, kuchukua tahadhari stahiki.