Tuesday , 23rd Dec , 2014

Rais Jakaya Kikwete ameridhia azimio la bunge la kumuwajibisha waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Prof Anna Tibaijuka kwa kukiuka maadili ya utumishi wa umma.

Prof Anna Tibaijuka

Rais Jakaya Mrisho Kikwete ametengua uteuzi wa waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi Prof. Anna Tibaijuka kutokakana na makosa ya ukiukwaji wa maadili ya utumishi wa umma hasa namna alivyopokea sehemu ya fedha za malipo ya Escrow huku akimweka kiporo waziri wa nishati na madini Prof. Sospeter Muhongo.

Rais Kikwete ameyasema hayo jijini Dar es salaaam alipokuwa akizungumza na wazee wa jiji hilo ambapo amesema serikali haina upungufu wa dhamira kwa yote yenye utekelezaji wa maazimio ya bunge ambapo amesema yanayohusu utekelezaji yatatekelezwa na yanayozungumzika yatazungumzwa.

Kuhusu suala la kumwajibisha waziri wa nishati na madini Prof Sospeter Muhongo Rais Kikwete ameagiza uchunguzi ufanywe na bado hajapata majibu ila ndani ya siku mbili hizi atafanya maamuzi baada ya kujiridhisha ili uamuzi atakaoutoa usiwe wa kumuonea yeyote.

Pia kuhusu kumuwajibisha Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, Amesema kuwa ameagiza uchunguzi ufanyike na akithibitika, taratibu za kuwajibisha watumishi wa umma zifuatwe chini ya mamlaka husika.

Kuhusu Bodi ya TANESCO, Rais amesema kuwa bodi hiyo tayari imemaliza muda wake, na hivi ipo katika mchakato wa kuundwa upya, na tayari amekwisha teua mwenyekiti mpya wa bodi hiyo.

Kuhusu mitambo IPTL amesema kuwa serikali haiwezi kukurupuka kuitaifisha mitambo hiyo kwa kuwa kitendo hicho kitawaogopesha wawekezaji katika kipindi hiki ambacho serikali inafanya jitihada mbalimbali kuvutia wawekezaji.

Aidha kuhusu pendekezo la kuwawajibisha Jaji Luhangisa na Jaji Mujurusi, Rais Kikwete amesema kuwa suala hilo amemuachia Jaji Mkuu alishughulikie kwa taratibu husika, na endapo muhimili huo wa mahakama utaridhika kuwa majaji hao wamepoteza sifa za kuendelea kuwa majaji, atawachukulia hatua.

Kuhusu wenyeviti wa kamati za bunge waliotajwa kuhusika katika sakata hilo, Rais Kikwete amesema kuwa suala hilo ameliachia Bunge liwashughulikie.

Kuhusu kuweka wazi mikataba ya umeme, amesema kuwa serikali imelichukua pendekezo la Bunge lakini haitakuwa sawa kuanika mikataba ya wawekezaji kwa kuwa kuna suala la SIRI katika kuingia mikataba hiyo, hivyo kuwalazimisha wawekezaji kuweka wazi mikataba baina yao na serikali ni sawa na kuwaogopesha wawekezaji kuwekeza Tanzania.

Rais Kikwete amesema kuhusu kuzitangaza benki za Stanbic na Mkombozi kuwa taasisi za utakatishaji fedha, uchunguzi zaidi utafanyika ili kubaini ukweli wa hilo.

Aidha Rais Kikwete katika hotuba yake hakusita kuwapongeza wabunge wote kwa kazi nzuri waliyoifanya na kwamba atamshangaa mbunge yeyote wa CCM ambaye alikuwa anatetea suala la Escrow.

Akizungumzia suala la uchaguzi wa serikali za mitaa ameeleza kuridhishwa na hatua zilizochukuliwa na waziri wa TAMISEMI Hawa Ghasia kuhusu watendaji waliohusika kuvuruga uchaguzi huku akiliagiza jeshi la polisi kuwachukulia hatua watu wote waliohusika na vurugu wakati wa zoezi hilo kwani mtindo huo wa vurugu ukiachwa uendelee utaleta athari kubwa katika uchaguzi mkuu ujao.

Awali akimkaribisha Rais, mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Bw. Said Meck Sadick amesema uchaguzi wa serikali za mitaa umefanyika kwa utulivu ambapo CCM imeshinda kwa asilimia 75, CHADEMA asilimia 14, CUF asilimia 11 ambapo amesema kwa matokea ya uchaguzi huo CCM bado inakubalika kwa wananchi.