Friday , 20th Jun , 2014

Wizara ya Nishati na Madini nchini Tanzania imethibitisha taarifa kuwa serikali ya Kenya imeomba msaada wa kuuziwa tani elfu kumi za mafuta ya ndege yanayojulikana kitaalamu kama JET A1.

Msemaji wa wizara ya nishati na madini Bi. Badra Masoud.

Msemaji wa wizara hiyo Bi. Badra Masoud amesema hayo leo jijini Dar es Salaam na kufafanua kuwa ombi hilo limetokana na Kenya kukumbwa na uhaba wa dharura wa mafuta hayo.

Bi. Masoud amesema Tanzania imeridhia ombi la Kenya kutokana na kuwa na hazina ya kutosha ya mafuta hayo na kwamba shehena ya kwanza imeshasafirishwa hii leo huku akifafanua kuwa uamuzi wa kuwapatia Kenya mafuta hayo ni sehemu ya kuimarisha ujirani mwema.

Hata hivyo, Bi. Masoud amesema shehena ya mafuta watakayouziwa Kenya ni ile ambayo haijapakuliwa na kukabidhiwa kwa makampuni husika kama taratibu za kampuni inayosimamia taratibu ya ununuzi wa mafuta kwa jumla yaani Petroleum Importation Coordinator au PIC.

Bi. Masoud ameondoa shaka juu ya uwezekano wa Tanzania kukumbwa na uhaba kama huo kwa maelezo kuwa Tanzania ina kiasi cha kutosha cha mafuta hayo.

Wakati huohuo, serikali nchini Tanzania kupitia Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na shirika la maendeleo la Japan JICA, wamefanya mapitio ya uboreshaji wa miundombinu ya umeme katika jiji la Dar es salaam na mkoa wa pwani.

Akizungumza leo jijini Dar es salaam, afisa habari wa wizara ya nishati na madini Bi. Badra Masoud amesema kwa sasa wanaangalia ni maeneo gani yenye matatizo ya miundombinu ya umeme ikiwa ni pamoja na maeneo yanayokuwa kwa kasi.

Aidha Bi. Masoud ameongeza kuwa pamoja na kurekebisha miundombinu hiyo pia wapo katika mchakato wa kuboresha vituo vya umeme kikiwemo cha Mbagala,na Kijitonyama ili viweze kutoa umeme wa uhakika.