Wednesday , 22nd Oct , 2014

Serikali ya Tanzania imesema kuwa katika kipindi cha miaka 18 hapajaripotiwa mgonjwa wa polio kutokana na kudhibiti magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid

Kauli hiyo imetolewa na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa wizara ya afya na Ustawi wa Jamii, Dk Neema Rusibamaila kwenye uzinduzi wa kampeni shirikishi ya chanjo ya surua- rubella iliyofanyika kitaifa katika viwanja vya mwalimu Nyerere mjini Dodoma.

Dk Rusibamaila amesema mwaka huu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inaendelea na mchakato wa kuitangaza Tanzania kuwa nchi iliyothibitika kutokuwa na ugonjwa wa polio.

Kwa upande wake waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kuwapeleka watoto wao kwenye vituo vya kutolea huduma ya chanjo ili kuwakinga na magonjwa yote yanayozuilika kwa chanjo ili kuboresha maisha ya watu na uchumi wao.