Wednesday , 23rd Dec , 2015

Serikali ya Tanzania imesema pamoja na kuzingatia amani inakuwepo katika nchi za Afrika Mashariki lakini pia itasimamia kupunguza makali ya soko la huria kwa nchi hizo ili kukuza uchumi wa wananchi wake.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga

Akiongea na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga amesema kupunguza makali hayo kutafanya kila mwananchi afaidike na Jumuiya hiyo.

Waziri Mahiga amesema kuwa kwa mujibu wa takwimu zinaonesha kuwa Tanzania baada ya miaka mitano ijayo itakuwa ni katika nchi zenye uchumi wa kati lakini kunatakiwa kuwepo uwiano wa maisha katika ukuaji wa uchumi huo.

Waziri Mahiga ameongeza kuwa pamoja na takwimu hizo kuonesha hivyo lazima Tanzania ifanye juhudi za makusudi kuwatoa wananchi wake kutoka pale walipo na kuelekea katika uchumi huo wa kati.

Aidha Dkt. Mahiga amesema katika kuingia katika soko hilo ni lazima nchi izingatie viwango bora vya bidhaa ambazo nchi itazalisha huku akisisitiza kuwa nchi itatoka kwenye kuuza malighafi na kuanza kuuza bidhaa zenyewe.