Sunday , 22nd Jun , 2014

Wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Tanzania wametishia kufanya mgomo usio na kikomo kushinikiza jeshi la polisi lieleze alipo mwenyekiti wa jumuiya ya wanafunzi wa elimu ya juu TAHLISO Musa Mdede.

Mkuu wa polisi nchini Tanzania IGP Ernest Mangu. Ofisi yake imetakiwa kueleza alipo rais wa jumuiya ya wanafunzi wa elimu ya juu nchini TAHLISO Musa Mdede, vinginevyo wanafunzi hao wataitisha mgomo wa nchi nzima.

Mdede ambaye pia ni Rais wa serikali ya wanafunzi wa chuo cha sayansi za afya na tiba Bugando, alitoweka Jumatano iliyopita, muda mfupi kabla ya kurejesha fomu ya kutetea nafasi yake.

Baadhi ya viongozi kutoka vyuo ambavyo ni wanachama wa TAHLISO wametoa tishio la kufanya mgomo huo jijini Dar es Salaam jana, ambapo wametoa muda wa saa ishirini na nne kwa jeshi la polisi kueleza alipo mwenzao vinginevyo wataitisha mgomo huo.

Kwa mujibu wa wawakilishi hao wa wanafunzi, wanahusisha tukio la kutoweka kwa mwenzao na sababu za kisiasa kutokana na kile walichoeleza kuwa ni msimamo mkali wa Mdede wa kuzuia TAHLISO isitumike kwa malengo ya kisiasa.