Sunday , 28th Feb , 2016

Waziri Mkuu mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa amesema serikali imetenga kiasi cha shilingi za Tanzania bilioni 1.65/- kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo kwenye vyuo vya walimu hapa nchini.

Mheshimiwa Majaliwa ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na walimu na watumishi wa sekta ya elimu kutoka wilaya zote za mkoa wa Mtwara uliofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Ualimu Mtwara.

"Serikali inatambua uhumimu wa mafunzo kwa vitendo katika vyuo vya ualimu na kwa sababu hiyo mwezi huu wa Februari tumetoa shilingi bilioni 1.65/- kwa vyuo vya ualimu 35 vya umma nchini ili kuwezesha wakufunzi na walimu wanafunzi kushiriki kikamilifu mafunzo kwa vitendo (Block Teaching Practice). Fedha hizo zitumike kulipia posho za kujikimu, nauli na ununuzi wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia," alisema.

Mapema, akizungumza na mamia ya wakazi wa Mtwara kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa mashujaa, Waziri Mkuu amesema serikali imedhamiria kuimarisha elimu na akawaonya wale wote wanaowaharibia elimu watoto wa kike.

"Tunataka watoto wa kike nchini wasome hadi elimu ya juu waje wawe watumishi wa umma hapo baadaye. Kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake huku tukikumbuka kaulimbiu ya Mama Salma Kikwete ya kwamba 'Mtoto wa Mwenzio ni wa kwako'," alisema na kuonya kuwa "Yeyote atakayemharibia mtoto wa kike masomo kwa kumrubuni na chips au pipi ajiandae kwenda Lilungu, (gereza la mkoa wa Mtwara)", amesema.