Friday , 9th Oct , 2015

Serikali imewaomba radhi wananchi kutokana na tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara na kuahidi kuwa tatizo hilo litakwisha Oktoba 20 mwaka huu baada ya kumaliza matengenezo ya mitambo ya kuzalisha umeme iliyopo hapa nchini.

Waziri wa Nishati na madini, George Simbachawene

Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Nishati na madini, George Simbachawene wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma.

Aidha Simbachawene amesema kuwa hali hiyo ya kukatika kwa umeme imesababishwa na mabwawa ya kuzalisha umeme nchini kukauka hali inayoilazimu serikali kulifunga bwawa la Mtera lililopo mkoani Dodoma kutokana na kukosekana kwa maji ya kuendeshea mitambo.

Hata hivyo amesema kuwa kwa sasa serikali imejikita kuzalisha umeme kwa kutumia gesi ambayo imeshafika Dar es salaam kutokea Mtwara japo gharama yake ni kubwa kuliko ile ya kuzalisha umeme kwa kutumia maji.