Monday , 1st Sep , 2014

Serikali imeanza ujenzi na utekelezaji wa Miradi 1,555 ya Maji nchi nzima katika jitihada za kukabiliana na hatimaye kumaliza tatizo la uhaba wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi.

Waziri wa Maji na Umwagiliaji nchini Tanzania Profesa Jumanne Maghembe.

Waziri wa Maji, Pro. Jumanne Maghembe amesema hayo mwishoni mwa juma wakati wa ziara ya Rais Kikwete Mkoani Dodoma na kuongeza kuwa Mradi wa Maji wa Chunyu ni moja ya miradi hiyo inayojengwa pote nchini.

Waziri Maghembe amesema kuwa kati ya miradi hiyo, miradi 230 tayari imekamilika na inatoa huduma ya maji kwa wananchi milioni mbili katika mikoa mbali mbali ya Tanzania.

Wakati huo huo, Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania imetoa tahadhari ya kuwepo kwa upepo mkali unaoambatana na mawimbi makubwa unaotarajiwa katika maeneo yote ya ukanda wa Pwani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mamlaka hiyo jana Jijini Dar es Salaam hali hiyo itatokea kuanzia majira ya saa sita mchana kuanzia kesho na kesho kutwa ambapo kutakuwa na upepo wenye kasi ya kilomita 40 kwa saa pamoja na mawimbi makubwa yanayozidi mita 2.0 katika ukanda wa Pwani

Maeneo yatakayoathirika ni Pwani ya mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba huku Wakazi wa maeneo yaliyotajwa wanashauriwa kuchukua tahadhari.

Mamlaka ya Hali ya Hewa imesema hali hii inatokana na kuimarika kwa mgandamizo mkubwa wa hewa katika maeneo ya kusini mwa Afrika hivyo kusababisha upepo mkali wa Kusi, mashariki mwa Pwani ya Tanzania.