Monday , 24th Jun , 2019

Tanzania imetia saini Mkataba wa kupatiwa fedha za Msaada wa Shilingi Bilioni 60 za kitanzania kutoka Serikali ya Watu wa China bila ya masharti yeyote, ambapo Serikali ya Tanzania itaamua matumizi yake katika miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi wake.

Mkataba huo umesainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi na Makamu Mwenyekiti wa Shirika la Kimataifa la Misaada ya Maendeleo la China Bw. Zhou Liujun.

Mazungumzo ya Mawaziri hao yalilenga kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia baina ya China na Tanzania sambamba na kuibua maeneo ya kipaumbele na kimkakati yatakayotekelezwa kwa ushirikiano baina ya China na Tanzania.

Maeneo hayo ni pamoja na upembuzi yakinifu kwa ajili ya upanuzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ili kuwa  Taasisi Mahiri ya Tiba ya Moyo Kusini mwa Jangwa la Sahara, ujenzi wa mabwawa ya kuzalisha umeme ya Ruhudji (megawatt 358) na Rumakali (megawatt 222) mkoani yaliyoko mkoani Iringa na Njombe ambayo yote kwa pamoja yatakuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa takribani megawati 580, pamoja na upembuzi yakinifu wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge railway) sambamba na ukarabati wa reli ya TAZARA.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi ameishukuru Serikali ya China sambamba na kueleza kuwa kipaumbele cha Tanzania ni kudumisha na kuendeleza mahusiano mazuri ya kidiplomasia,kisaiasa na kiuchumi yaliyopo baina ya Nchi hizo mbili kwa manufaa ya pande zote mbili.