Thursday , 29th Jan , 2015

Serikali imesema itafanya uchunguzi kubaini ukweli wa madai ya matumizi makubwa ya nguvu kufanywa na polisi wakati wa kutawanya maandamano ya chama hicho Januari 27, mwaka huu, jijini Dar es salaam

Waziri wa mambo ya Ndani Mathias Chikawe

Serikali kupitia kwa Waziri wa mambo ya Ndani Mathias Chikawe imeagiza tume ya haki za binadamu na utawala Bora pamoja na Idara ya malalamiko ya wizara hiyo, kufanyia uchunguzi madai kuwa Jeshi la Polisi lilitumia nguvu kubwa kupita kiasi wakati wa kutawanya maandamano ya wafuasia wa CUF.

Madai mengine yanayopaswa kuchunguzwa ni matumizi ya silaha zisizostahili ikiwemo 'Spana' ya matairi ya gari katika zoezi la kutawanya maandamano hayo yaliyokuwa yakifanywa na wafuasi wa CUF wakiongozwa na Mwenyekiti wao Prof. Ibrahim Lipumba.

Serikali pia imewaomba radhi wananchi wote waliokumbwa na kadhia ya mabomu na vipigo kutoka kwa polisi katika maandamano hayo yaliyofanywa juzi Mbagala Jiji Dar es Salaam ambao hawakuhusika na maandamano hayo.

Akitoa tamko la serikali bungeni kuhusiana sakata hilo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Mhe. Mathias Chikawe, amesema kilichotokea juzi na wafuasia wa chama hicho ni uvunjaji wa sheria kwa makusudi katika kutaka umaarufu wa kisiasa na huruma ya wananchi.

Kwa upande wake, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kupitia kwa mkurugenzi wake Dokta Hellen Kijo-Bisimba, kimekemea vitendo hivyo ilivyodai kuwa ni ukiukwaji mkubwa wa sheria, kutokana na matakwa ya baadhi ya viongozi wasio waaminifu serikalini na ndani ya jeshi la polisi.

Katika hatua nyingine serikali imetakiwa kubadili mfumo wa utendaji kazi  wa jeshi la polisi nchini kutokana na kuwa na mifumo ya kikoloni na ukandamizaji jambo linalolifanya jeshi hilo kutenda shughuli zake kwa kukiuka haki za binadamu.

Hayo yamesemwa bungeni mjini dodoma na baadhi ya wabunge wakati wakichanga mjadala wa hoja ya dharura iliyowasilishwa bungeni na Mh. James Mbatia kufuatia tukio la kupigwa kwa mwenyekiti wa chama cha wananchi.
 
Aidha baadhi ya wabunge wamemtaka waziri mkuu kuliomba bunge radhi pamoja na watanzania wote na kisha kufuta kauli yake aliyoitoa bungeni inayodaiwa kuhamasisha polisi kupiga raia sambamba na waziri wa mambo ya ndani Mh. Mathias  Chikawe kujiuzulu nafasi yake.
 
Pia wamependekeza kuwajibishwa kwa baadhi ya polisi waandamizi walioshiriki katika matukio mbalimbali yaliyosababisha mauaji na majeraha kwa wananchi badala ya kuwapandisha vyeo pamoja na kuweka mifumo itakayolifanya jeshi hilo kuwa huru badala ya kuwa jeshi la kupokea maagizo.