Sunday , 26th Aug , 2018

Mwanasiasa mkongwe na maarufu Marekani Seneta John McCain, amefariki dunia jana Agosti 25, 2018 akiwa na umri wa miaka 81.

Marehemu John McCain.

McCain ambaye anawakilisha jimbo la Arizona kwa miaka 30 amekutwa na mauti baada ya kusumbuliwa na saratani ya ubongo ambayo iligundulika mwaka 2017 wakati madaktari walipomfanyia upasuaji kuondoa damu iliyokuwa imeganda  juu ya jicho lake la kushoto.

Mbali na ushiriki wake kwenye siasa McCain anaheshimika kama mmoja wa mashujaa wa vita.
Katika vita vya Marekani na Vietnam, Seneta McCain, alikuwa mmoja wa wanajeshi wa jeshi la anga la Marekani na katika moja ya mashambulizi yake ya ndege akiwa kama rubani alidunguliwa na wapiganaji wa Vietnam na kudondoka kisha yeye kushikiliwa kama mateka wa vita kwa zaidi ya miaka mitano.

McCain aliwahi kuwania kupata tiketi ya kuwa mgombea Urais kupitia chama cha Republican mwaka 2000 ambapo alishindwa na Rais George Bush. Aliingia tena kwenye kinyanganyiro hicho mwaka 2008 na kufanikiwa kuwa mgombea kwa tiketi ya chama cha Republican na kushindwa na aliyekuwa Rais Barack Obama.    

Seneta McCain alifanya mambo mengi ya kihistoria na katika awamu ya Rais Donald Trump atakumbukwa kwa uthubutu wake wa kupinga matendo na mapendekezo yaliyoletwa na serikali.