Wednesday , 3rd Sep , 2014

Kukosekana kwa vyombo vya usimamizi na kuratibu maendeleo ya mtoto kumetajwa kuwa ni sababu ya kuongezeka kwa vitendo vya ukatili kwa watoto ikiwemo suala la ndoa za utotoni.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Bi. Sophia Simba. Waziri Simba wizara yake ndiyo yenye jukumu la kusimamia ulinzi wa haki za watoto nchini Tanzania.

Akizungumza na East Africa Radio Mkurugenzi wa kituo cha Msaada wa sheria kwa wanawake na watoto (WILAC) Theodosia Muhulo amesema changamoto iliyopo mbali na kuwepo na sheria ya kumlinda mtoto ni kukosekana kwa vyombo maalumu vya ufuatiliaji wa vitendo hivyo kuanzia majumbani ili kubaini wale wanaotenda kinyume na sheria.

Hata hivyo Bi Muhulo amesema ipo changamoto kubwa hasa katika sheria ya ndoa na ya umri wa mtoto na kueleza kuwa ni vyema sheria hizo kufanyiwa marekebisho kwa kuwa sheria hizo zimepitwa na wakati.

Wakati huo huo, serikali imeitaka wakala wa usalama na afya mahali pa kazi (Osha) kuhakikisha kuwa inaorodhesha na kutambua maeneo yote ambayo hayajasajiliwa ili waweze kuyasajili na kuwapatia vyeti.

Kauli hiyo imetolewa jana na Waziri wa kazi na ajira, Gaudensia Kabaka wakati akizindua mkataba wa huduma kwa mteja ulioandaliwa na Osha wenye lengo la kuongeza tija mahali pa kazi mjini Dodoma.

Aidha Waziri Kabaka ameitaka Osha kutoa huduma zote muhimu kwa ajili ya kuhakikisha kuwa afya za wafanyakazi zinakuwa salama hasa kwa wafanyakazi wa viwandani na wale wanaotengeneza kemikali.