Thursday , 18th Jun , 2015

Zoezi la uandikishaji katika daftari la kudumu la wapiga kura mkoani Morogoro limeingia dosari baada ya kushindwa kuanza rasmi siku ya Jumatatu kutokana na kukosekana vifaa na kusababisha wasiwasi mkubwa kwa wananchi kukosa haki ya kupiga kura.

Foleni ya mawe yalipangwa kwa namba na majina na wananchi kwa lengo la kushika nafasi

Zoezi la uandikishaji katika daftari la kudumu la wapiga kura mkoani Morogoro limeingia dosari baada ya kushindwa kuanza rasmi siku ya Jumatatu kutokana na kukosekana vifaa na kusababisha wasiwasi mkubwa kwa wananchi kukosa haki ya kupiga kura.

Eatv imeshuhudia vituo mbalimbali vya kuandikisha wapigia kura vikiwa vimefungwa huku wananchi waliojitokeza wakiwa wamepanga mawe kwa namba na majina wakimaanisha kushika nafasi baada ya zoezi la uandikishaji kuahirishwa kutokana mashine kukosa wino

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wameeleza wasiwasi wao kuwa muda wa kuandikisha ni mdogo na mwitikio wa wananchi katika zoezi hilo ni mkubwa.

Naye afisa mtendaji wa kijiji cha Kigugu wilaya ya Mvomero amesema anashangazwa na hatua ya tume ya uchaguzi kushindwa kuandaa vifaa vya kutosha na badala yake wananchi wanakata tamaa kutokana na kutokuwepo taarifa sahihi za uandikishaji.

Kwa upande wake afisa uandikishaji manispaa ya Morogoro Pascal Mayala amepinga taarifa zinazotolewa na watu kuwa zoezi limeahirishwa na badala yake tume ilipanga zoezi hilo kuanza rasmi Juni 20 vifaa vitakapokuwa vimekamilika ambapo amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha.