Tuesday , 26th Aug , 2014

Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu nchini Tanzania Mh. Benjamini William Mkapa amesema tatizo la maadili kwa viongozi na watumishi wa umma halijapewa uzito unaostahili katika kulidhibiti na hivyo kusababisha wananchi kukosa huduma muhimu na za msingi.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu nchini Tanzania, Mh. Benjamin William Mkapa.

Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam, Mh. Mkapa amesema tatizo la mgongano wa kimaslahi miongoni mwa viongozi na watumishi wa umma limekuwa likijitokeza mara kwa mara hasa kwa wale wenye mamlaka au watoa maamuzi serikalini wanapokuwa na maslahi katika jambo fulani wanatumia madaraka waliyonayo kuendeleza maslahi yao binafsi badala ya kutoa kipaombele kwa maslahi ya umma.

Kutokana na tatizo Mh. Mkapa ameitaka sekretarieti ya maadili ya umma ya viongozi kuharakisha mchakato wa upatikanaji wa sheria ya kudhiti tatizo hilo ambalo amesema kama halitatafutiwa ufumbuzi wananchi wanyonge wataendelea kukosa haki zao za msingi kutokana na ubinafsi wa viongozi.

Katika hatua nyingine, Msururu wa michango na gharama zinazotozwa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, imefanya gharama ya elimu katika shule za umma katika manispaa hiyo kuwa za juu kuliko hata gharama zinazotozwa na shule binafsi ambazo elimu ni ya kulipia.

Hayo yamebainishwa leo wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa hiyo, ambapo mmoja wa wake ambaye bunge wa Kawe Bi Halima Mdee ameutaka uongozi wa Manispaa hiyo kufafanua ni vipi inasimamia sera ya serikali ya elimu bure na kwamba ikibidi itaje kiwango halisi ambacho wazazi wanapaswa kulipa kwa ajili ya watoto wanaosoma kwenye shule za umma.

Kwa mujibu wa mbunge Mdee, baadhi ya walimu na kamati za shule zimekuwa hazitumii ipasavyo michango na gharama hizo, na kwamba katika nyakati fulani baadhi ya walimu wamekuwa wakitumia fursa hiyo kujinufaisha wenyewe kupitia msururu wa ada na michango aliyoitaja kuwa ni mzigo kwa wazazi.