Rais Kikwete leo amezindua miundombinu ya kuchakata na kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara na Songo Songo hadi Dar es Salaam kupitia Somanga, katika hafla iliyofanyika katika eneo la Madimba mkoani Mtwara.
Katika hotuba yake Rais Kikwete amesema uzinduzi huo ni hatua muhimu kuelekea katika taifa lenye uchumi wa kati kwa kuimarisha huduma za nishati ya umeme pamoja na uchumi katika Nyanja mbalimbali ikiwemo viwanda kwa kuwa gesi hiyo itamaliza kabisa tatizo la umeme.
Katika uzalishaji wa umeme, Rais Kikwete amewaagiza watendani wa shirika la umeme nchini TANESCO na lile la mafuta TPDC kuwa makini katika mchakato wa manunuzi kwa kufuata sheria ili matatizo yaliyowahi kulikumba taifa hili kutokana na ukiukwaji wa taratibu mwaka 2006 yaliyosababishwa na uhaba wa umeme, yasijirudie tena.
Rais Kikwete licha ya kuishukuru serikali ya China kuwa tayari kujenga miundombinu hiyo, ameziagiza mamlaka husika kuhakikiksha kwamba zinatoa huduma muhimu za jamii ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa maji safi na salama, pamoja na barabara kwa wakazi wa Mtwara ili wanufaike na gesi hiyo.
Awali akitoa maelezo ya utangulizi, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) Tanzania Dkt. James Mataragio ameeleza kuwa miundombinu hiyo imekamilika na tayari gesi imeshaanza kusukumwa kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.
Dkt Mataragio amesema kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo umegharimu dola za kimarekani bilioni 1.53 sawa na trillion 2.926 za kitanzania ikiwa ni pamoja na gharama ambazo hazikuwa ziko nje ya gharama halisi ya miundombinu hiyo.
Amesema kuwa asilimia 95 ya gharama hizo zinatokana na mkopo kutoka Benki ya Exim ya China huku asilimia 5 ikitoka serikalini.
Akizungumzia faida za miundombinu hiyo, Dkt Mataragio ametaja faida kadhaa za gesi hiyo ikiwa ni pamoja na kutumika katika uzalishaji wa umeme jambo litakaloifanya Tanzania kuwa na umeme wa uhakika.
Ametaja faida nyingine kuwa ni pamoja na kuongeza pato la taifa kutokana na uuzaji wa gesi hiyo nje ya nchi, kuokoa fedha za kigeni ambazo hutumika kuagizia mafuta kutoka nje ya nchi, kukuza uchumi kupitia ukuzaji wa sekta ya viwanda, kuongeza mapato ya halmashauri kupitia mirabaha pamoja na kuchochea utafiti wa mafuta na gesi.
Amesema miundombinu hiyo itakuwa na uwezo wa kusukuma futi za ujazo milioni 784 kwa siku ifikapo mwaka 2020, ambapo kwa sasa inasukuma futi za ujazo milioni 80 pekee.
Akimkaribisha Rais Kikwete, waziri wa Nishati na madini George Simbachawene, amesema kuwa huo ni utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi, na kwamba serikali ina mpango wa kujenga mitambo ya umeme mkoani Mtwara itakayozalisha zaidi ya Mega Watt 600 kwa ajili ya mikoa ya kusini.
“Mheshimiwa Rais tunakupongeza sana kwa jitihada zako, kuna watu wanabeza wanahoji eti utatuachaje, mimi nawaambia kwamba ulipoingia ulitukututa na gesi ya futi za ujazo trillion 8, lakini unatuacha na futi za ujazo trillion 52”, amesema Simbachawene na kuongeza kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo utazalisha ajira zaidi ya 1363 katika eneo hilo la Mtwara.